Fungamaneni na Maisha ya Mtume SWA

Religious

Waumini wa Dini ya Kiislamu popote walipo katika kipindi hichi cha kusherehekea uzawa wa Kiongozi wa Dini hiyo Ulimwenguni Mtume Muhammad { SAW } wana wajibu wa kupitisha maazimio ndani ya nafsi zao ya kuachana na maovu na kukumbatia mema yote kama alivyokuwa akiyahubiri Kiongozi huyo wakati wa uhalifa wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika kisomo cha mazazi ya Mtume Muhammad { SAW } kilichofanyika katika ukumbi wa wapenzi wa Mtume Muhammad { SAW } wa Chaurembo waliopo katika Mtaa wa Msimbazi Kariakoo Mjini Dar es salaam.

Balozi Seif alisema mkusanyiko wa waumini wa Kiislamu katika kutukuza uzawa wa Kiongozi wao utakuwa na manufaa makubwa endapo kila muumini atadhamiria kusoma kwa kina maisha ya kiongozi huyo kwa lengo la kufuata mwenendo wake.

Alitoa wito kwa wapenzi wa Mtume Muhammad { SAW } kufanya utafiti mbali mbali zitakazotoa fursa kwa waumini wa dini ya Kiislamu popote pale kusoma na hatimae kuelewa vyema maisha na mfumo aliokuja nao Kiongozi huyo wa umma wa Kiislamu.

“Ikiwezekana tafiti hizo ni vyema zikaandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili watu wengi zaidi wapate kuzisoma. Kuelewa maisha ya Mtume Muhammad { SAW } ni hatua muhimu kwa muumini wa Kiislamu kuielewa Dini yake “. Alisisitiza Balozi Seif.

” Akinukuu baadhi ya maandiko yaliyotolewa na wanafalsafa wa Dini ya Kiislamu Balozi Seif alisema kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad { SAW } ni sawa na kusherehekea kuzaliwa kwa Uislamu”.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasisitiza waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kuwa na utiifu, subra wakati wa matatizo sambamba na kujijengea maisha bora ya milele ambayo kila muumini anayaelewa.

Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na uwepo wa Umoja wa wapenzi wa Mtume Muhammad { SAW } hapa Tanzania ambao unastahiki kupongezwa pamoja na kuungwa mkono.

Alisema jamii katika kipindi kirefu ilikuwa ikishuhudia kuwepo kwa umoja wa wapenzi wa vilabu vya mchezo wa mpira wa miguu au wanamuziki badala ya kuwa na umoja kama huo unaoleta faida pande zote mbili Duniani na Makazi ya milele.

“Maandalizi ya sherehe hiziyameonyesha wazi kwamba nyinyi kweli ni wapenzi wa Mtume Muihammad { SAW }. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuzidishie mapenzi yetu kwa kiongozi wetu huyo”. Alifafanua Balozi Seif.

Akitoa salamu kwenye hafla hiyo ya kisomo cha mazazi ya Mtume Muhammad { SAW } Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi alisema waumini wa Dini ya Kiislamu wana wajibu wa Kumshukuru Mola kwa kuupatia umma huu wa mwisho Kiongozi aliyekamilika kwa tabia, nasabu pamoja na Umbo.

Mzee Mwinyi aliwataka waislamu hao kuendelea kuheshimu nema walizopewa na Mwenyezi Mungu za kupatia Kitabu kitukufu na bora chenye mfumo kamili wa kufuatwa na wanaadamu katika maisha yao ya kila siku.

Mapema Mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu kilichopo Tandika Mjini Dar es salaam akiwa miongoni mwa matunda ya chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu cha Al – Akhzal nchini Misri Sheikh Usama Ismail alisema dalili za utukufu wa Mtume Muhammad { SAW } zilianza kujichomoza tokea zama za Mitume waliomtangulia.

Sheikh Usama alifahamisha kwamba Kiongozi huyo wa Umma wa Kiislamu alibashiriwa utukufu wa kuja kwake duniani ambao baadhi ya maulamaa wa enzi zilizopita waliushuhudia ndani ya vitabu vitukufu.

Katika hafla hiyo ya kisomo cha mazazi ya Mtume Muhammad { SAW } Muasisi wa Umoja wa wapenzi wa Mtume Muhammad { SAW } wa Chaurembo waliopo katika Mtaa wa Msimbazi Kariakoo Sheikh Majid aliwapongeza Viongozi hao kwa ukaribu wao na waumini pamoja na wananchi kwenye masuala mbali mbali ya kijamii.

Katika kuunga mkono harakati za kijamii zinazofanywa na viongozi hao Sheikh Majid kwa niaba ya Umoja huo alikabidhi zawadi za Juzuu, Mashafu pamoja na hati maalum kama ukumbusho kwa wageni hao waalikwa akiwemo pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al Hajj Daktari Ali Mohamed Shein.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar